Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema kuwa amefikia makubaliano na mgombea urais wa chama cha Democrat Kamala Harris kushiriki mdahalo wa televisheni Septemba 10, siku mbili tu baada ya kutishia kujiondoa.
Hata hivyo hakukuwepo uthibitisho juu ya maafikiano hayo kutoka kwa makamu wa rais Kamala Harris.
Donald Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth kwamba wapinzani hao wamekubaliana kuwa mdahalo huo kwenye kituo cha televisheni cha ABC News utaendeshwa chini ya sheria sawa na mdahalo wa kituo cha CNN uliofanyika mnamo Juni 27, bila kuwepo watu jukwaani na kipaza sauti cha kila mgombea kuzimwa wakati mwenzake anapozungumza.
Licha ya kukishtumu kituo cha televisheni cha ABC News kwa kuna na upendeleo, Trump amesema kituo hicho kimempa hakikisho kwamba mdahalo huo utakaofanyika mjini Philadelphia, utaendeshwa kwa njia ya haki na usawa.