Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, ameikosoa vikali hatua ya Rais Joe Biden kuruhusu Ukraine kutumia silaha za Marekani kushambulia maeneo ya ndani ya Urusi, akitaja uamuzi huo kuwa “wa kijinga.”
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makazi yake ya Mar-a-Lago, Trump alisema hakushauriwa kuhusu hatua hiyo licha ya kuwa atachukua madaraka Januari 20. Trump aliongeza kuwa anaweza kufikiria kuibatilisha hatua hiyo mara atakapoingia madarakani.
Biden alitoa ruhusa hiyo mwezi uliopita, akiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kushambulia maeneo ya Urusi, hatua iliyochukuliwa baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa Rais Volodymyr Zelenskyy na washirika wa Magharibi.
Hata hivyo, Ikulu ya Marekani ilitetea uamuzi huo, ikisema ulifikiwa baada ya mashauriano ya miezi kadhaa. Msemaji wa usalama wa taifa, John Kirby, alisema maelezo ya kina kuhusu mantiki ya uamuzi huo yalitolewa kwa timu ya Trump baada ya uchaguzi.
Trump, ambaye mara nyingi amekuwa akilaumiwa kwa msimamo wake wa karibu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesisitiza kuwa anaweza kuleta suluhu ya haraka kati ya Ukraine na Urusi, ingawa alikiri kuwa mgogoro huo unaweza kuwa mgumu zaidi kuutatua kuliko changamoto za Mashariki ya Kati.