Rais mteule wa Marekani Donald Trump amependekeza Israel na Hamas wanaweza kukubaliana kusitisha mapigano Gaza mwishoni mwa wiki hii.
Mazungumzo kati ya wawakilishi wa Israel na Hamas yameanza tena katika mji mkuu wa Qatar Doha hii leo, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuashiria kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yapo ukingoni hapo jana.
Kiongozi huyo wa Marekani anayemaliza muda wake alisema itajumuisha makubaliano ya kuwaachilia mateka na “kuongezeka” kwa misaada kwa Wapalestina, katika hotuba yake ya mwisho ya sera ya kigeni kama rais.
“Watu wengi wasio na hatia wameuawa, jamii nyingi zimeharibiwa. Wapalestina wanastahili amani,” alisema.
“Mkataba huo ungewakomboa mateka, kusimamisha mapigano, kutoa usalama kwa Israeli, na kuturuhusu kuongeza kwa kiasi kikubwa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina ambao waliteseka vibaya katika vita hivi ambavyo Hamas ilianzisha.”
Wapatanishi wa Qatar wametuma Israel na Hamas rasimu ya pendekezo la makubaliano ya kusitisha mapigano.
Wapatanishi wa Marekani na Waarabu walifanya maendeleo makubwa mapema wiki hii kuelekea kusuluhisha usitishaji mapigano katika vita vya Israel na Hamas na kuachiliwa kwa mateka wengi walioshikiliwa katika Ukanda wa Gaza – lakini makubaliano bado hayajafikiwa, maafisa walisema.