Kaimu mkurugenzi mtendaji wa tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt.Catheren Joachim amesema serikali ya Tanzania itaendelea kulinda usalama wa wananchi kwa kuhakikisha wanaendelea kuwa na afya huku akiwatoa hofu watumiaji wa ARVs kwa kuwa serikali itahakikisha upatikanaji wa dawa hizo za kuongeza kinga za mwili unakuwa endelevu.
Dkt.Catheren ameeleza hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada kongamano la kujenga uelewa wa masuala ya ya VVU na Ukimwi kwa vijana Balehe wa shule za msingi na sekondari wa mkoa huo ambapo amesema kupitia vyombo vya habari TACAIDS wameona taarifa inayoelezea juu ya uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha misaada kwa mashirika ya afya huku akibainisha kuwa hakuna taarifa waliyopokea lakini serikali itaendelea kulinda usalama wa wananchi.
“Na sisi pia tumeliona kwenye vyombo vya habari kwa hiyo tunasubiri taarifa rasmi lakini tunaimani serikali bado itaendelea kulinda usalama wa wananchi lakini napenda niwahakikishie bado serikali inafanya jitihada mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya kwa hiyo sidhani kama itatokea athari ya aina yoyote kwa hiyo niwaombe tuwe na subira kwasababu serikali haijatoa tamko rasmi”amesema Dkt.Catheren
Kupitia ukurasa wa X (zamani Twitter) Waziri wa zamani wa ardhi,Prof.Anna Tibaijuka amesema afya za mamilioni ya Waafrika na Watanzania zipo hatarini kutokana na uamuzi huo huku akishauri wizara ya afya kuufahamisha umma ni hatua gani za haraka zinahukuliwa kutathmini jambo hilo na kuchukua hatua stahiki kwa kuwa upatikanaji wa dawa za kuongeza kinga za mwili ARVs utaathirika.