Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, amefanya mkutano wake wa kwanza baada ya kutoka Ikulu ya White House na kuzungumzia suala la kuhesabiwa kwa kura katika uchaguzi uliopita huku akikosoa sera za Rais Joe Biden na Chama cha Democrats.
Akiwahutubia maelfu ya watu huko Wellington, Ohio, Trump alisisitiza madai yake kwamba kushindwa kwake katika uchaguzi wa Novemba 2020 kulisababishwa na ulaghai kwenye kuhesabu kura na kusema, “Tulishinda uchaguzi mara mbili na tunaweza kuhitaji kushinda mara ya tatu. Inawezekana.”
Kwenye mkutano huo, ambapo Donald Trump hakutoa taarifa wazi kuhusu iwapo atagombea tena au la, alitoa maneno ya kutia moyo kwa wapiga kura kwamba Chama cha Republicans kinaweza kupata tena idadi kubwa ya wanachama kwenye Baraza la Seneti la Marekani na Baraza la Wawakilishi.
Trump aliongezea kusema, “Tutachukua tena Bunge, Seneti na Utawala wa Marekani, tutafanya hivyo hivi karibuni.”