Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora imefanya Kikao Maalum na Waandishi wa Habari Mkoani Iringa Kwa lengo la kuelezea namna Tume hiyo inavyofanya kazi na namna ilivyoshughulikia baadhi ya Kesi na matukio yaliyoripotiwa Kupitia Vyombo vya habari juu ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu na matumizi mabaya ya nguvu ya Uongozi na Mamlaka ya kiutawala Nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Kikao hicho kilichofanyika Februari 18, 2025 katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano uliopo Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Dkt.Thomas Masanja, amesema Tume hiyo itafanya kazi mkoani Iringa Kwa Siku 20 kuanzia (Februari 17, 2025 hadi Machi 07,
2025) ambapo inatarajia kutoa elimu kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Watendaji wa Vijiji na Mitaa, Wakazi na Wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo katika maeneo mbalimbali katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwawezesha kutambua haki zao na kudumisha utawala unaozingatia haki za binadamu.
Dkt. Masanja ameeleza kuwa zoezi hilo litaambatana na kutembelea Magereza za Mkoa wa Iringa kwa lengo kukagua na kutathmini haki za watu wanaozuiliwa, na kutoa mapendekezo jinsi ya kutatua matatizo yaliyopo kwa mujibu wa taratibu na Sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kukagua viwango vya kimataifa na kikanda vinavyolinda na kutetea haki za binadamu ikiwemo makundi ya watu waliozuiliwa.
“Sisi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora kwa kulinganisha na mahakama, Tume haitoi Amri (Order), inachokipata kutokana na matokeo ya uchunguzi, tunatoa mapendekezo ya nini kifanyike Kwa Mamlaka inayohusika, lakini Sheria na katiba vinaipa nguvu Tume kufuatilia mapendekezo yake” –
Amesema Dkt. Thomas Masanja.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora ni idara Huru ya Serikali iliyoandishwa kama Taasisi ya Kitaifa iliyopo kitovu cha Kukuza na kulinda haki za binadamu na Utawala Bora Nchini Tanzania.