Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka amewaasa vijana waliopo kwenye Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT – Life) kufanya vizuri zaidi kwa kutumia fursa waliyopata ili kufikia malengo ya Serikali.
TUMIENI VIZURI FURSA YA BBT MFIKIENI MAONI YA RAIS SAMIA
Mhe. Balozi Kusiluka amebainisha hayo leo (07.08.2023) katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane), kushuHUdia kwa vitendo maendeleo ya programu hiyo.
Amewataka vijana hao ambao wapo kwenye programu ya BBT – LIFE kwa vitendo katika unenepeshaji wa ng’ombe, kaa na jongoo bahari pamoja na ulimaji wa zao la mwani, kufikia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameasisi programu hiyo ili kuwezesha vijana kiuchumi.
Ameongeza kuwa ameridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na vijana hao na kuwataka kuongeza jitihada zaidi kufikia maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo ni vyema wakatumia vizuri fursa waliyoipata.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe amesema wizara imeweka mpango maalum kwa vijana hao baada ya kumaliza mafunzo kwa kuwapatia maeneo kwa mkataba wa miaka mitano pamoja na mtaji watakaokuwa wamepata wakati wa mafunzo ili kuendeleza biashara ya kunenepesha ng’ombe.
Naye mmoja wa wanufaika wa programu ya BBT – LIFE Sekta ya Mifugo, Bi. Rest Mgonja amesema wameshiriki kwa kupewa maeneo na mitaji pamoja na kununua ng’ombe ambapo kila kijana alipatiwa ng’ombe kumi na kuwa na jumla ya ng’ombe 2,400 kwa vijana 240 kwa ajili ya kunenepesha na kuwauza baada ya miezi mitatu, ambapo tayari wameuza ng’ombe 565.
Kwa upande wake mmoja wa wakufunzi wa wanufaika wa BBT – LIFE Sekta ya Uvuvi Bw. Hamisi Salehe amemuelezea Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Kusiluka namna wanavyotoa mafunzo kwa wanufaika jinsi ya kunenepesha viumbe maji wakiwemo kaa na jongoo bahari kwa kuyaongezea thamani mazao hayo na kuuzwa kwa thamani ya juu zaidi.