Ikiwa kama sehemu ya Kampeni yake ya kuhamasisha watanzania kutunza mazingira kwa kupanda miti 1,000,000 nchini kote, Kampuni ya Bayport imepanda miti ya matunda 500 katika Shule ya Sekondari Mapinduzi day na shule ya msingi Muungano wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, huku Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Vicent Mashingi akitoa wito kwa shule zote kupanda miti ili kukabiliana na changamoto za tabia nchi.
“Natoa shukurani zangu nyingi kwa Kampuni ya Bayport, tulishasema ‘soma na mti’kila mtoto shuleni walau awe na mti mmoja, tuchagua tupande miti ama tuache kuendesha magari, magari yanatoa hewa ya ukaa, mashine na viwandavonatoa hewa ya ukaa, vinachafua mazingira, chombo pekee kinachoweza kutoa hewa hiyo ni miti katika anga letu na kurudisha hali ya mvua, bila miti hatuwezi kuwa na kilimo bora”; alisema Dk. Mashingi akiongeza kuwa suala upandaji miti pia lipo kisheria.
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Bayport Tanzania, Bwana. Nderingo Materu alisema kampeni hiyo ya kupanda miti waliyoanza Temeke jijini Dar es Salaam Septemba mwaka huu, licha ya kuhamasisha jamii ya watanzania kuona umuhimu wa kupanda miti, bali wanafanya hivyo pia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mikakati na sera zake endelevu za uhifadi na usimamizi wa mazingira.
Alisema Kupungua kwa misitu kwa sababu ya uvunaji misitu usiokuwa endelelevu, ongezeko la shughuli za viwanda duniani, kupungua kwa theluji, mabadiliko ya utaratibu wa mvua , mafuriko, na ukame miongoni mwa jamii nyingi ulimwenguni umekuwa ukisababisha athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.
“Ili jamii yetu kujinusuru kutoka kwenye changamoto hizi zinazosabanishwa na mabadiliko ya tabia nchi tumeamua kuungana na Serikali kwa kusikiliza kusikiliza ushauri wataalam wa Mazingira kutoka NEMC kupanda miti Kwa wingi katika jamii zetu ili kuokoa maisha ya viumbe hai wengine pamoja na binadamu”
“Bayport Financial Services Tunatoa shukurani za dhati kwa wale wote waliosaidia kwenye kampeni hii ya kupanda miti 500 hapa Serengeti hususani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Afraha Hassan, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ayubu Mwita na Bwana Charles Butonesha kutoka taasisi inayoshughulika na uhifadhi wa mazingira na maliasili wilayani humo.
“Hatuwezi kuwasahau watoto na walimu wote wa shule hizi mbili, kwani wao ndio watakaohusika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha miti hii inaendelea, sisi kama Bayport tutakuwa mstari wa mbele katika kushiriki kampeni mbalimbali za uhifadhi wa mazingira ili nchi yetu iwe mahali salama pa kuishi kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchini”, aliongeza Bwana Materu.
Aidha Mugae Mwita King’ae mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mapinduzi alisema kuwa awali miti mingi iliyopandwa shuleni kwao ilikuwa ya kivuli lakini sasa wanaishukuru Bayport kwa kuwaletea miti ya matunda itaayowapa kivuli na lishe.