Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kuibua mbinu mpya zitakazoiwezesha Sekta ya Misitu na Nyuki kuongeza mapato katika pato la Taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro alipofanya kikao na menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.
“Tunategemea tuje na mbinu zote za kuongeza mchango wa Sekta ya Misitu na Nyuki kwenye uchumi wa nchi na mojawapo ya mchango huo ni biashara ya hewa ya ukaa (Forest Carbone Trade)”
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ina mamlaka kamili kwenye kusimamia biashara ya hewa ya ukaa kwa sababu sheria na sera ya misitu iko chini ya Wizara hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameishauri menejimenti ya TFS kuhakikisha inatekeleza mpango wa biashara ya hewa ya ukaa kwa wakati kwa sababu kwa kufanya hivyo itasaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya maliasili na utalii.
Pia, amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa kasi ili kuleta matokeo chanya.
“Tuendane na kasi ya utekelezaji wa mpango huu kwa sababu sisi tunapimwa pale tunapoonyesha matokeo chanya kama alivyosema Waziri tunaangaliwa tumeingiza fedha kiasi gani na watalii kiasi gani” Masanja amesisitiza.
Naye, Mtendaji Mkuu, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amewapongeza kwa kuteuliwa kwa mara nyingine kuiongoza Wizara na kuahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.