Wataalamu wa kimataifa katika sekta ya afya wanaamini kwamba wimbi la magonjwa katika eneo la mbali la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo ilikuwa imepewa jina la “Disease X”, limesababishwa na vimelea vya maradhi mbalimbali katika maeneo hayo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lenye makao yake makuu huko Geneva, Uswisi limesema kuwa malaria, virusi vya korona na vingine vinavyojulikana vimepatikana katika sampuli 430 za maabara zilizochukuliwa kutoka kwa wagonjwa kadhaa kutoka katika eneo hilo.
Matokeo ya uchunguzi yanaonesha kuwa mchanganyiko wa maambukizi ya virusi ya kawaida na yale ya mfumo wa upumuaji, malaria ikujumuisha na utapiamlo mkali kunasababisha kuongezeka kwa maambukizi makubwa na vifo na hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Tangu mwishoni mwa Oktoba, mamia ya watu walikumbwa na maradhi hayo katika wilaya ya Panzi, iliyoko kusini magharibi mwa jimbo la Kwango.
Waathirika walikuwa na dalili za mafua, ikiwa ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, kuuma viungo na tatizo la kupumua.