Jeshi la Uganda limesema kuwa limemuua kiongozi mkuu wa waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) waliohusika na mashambulizi ya hivi karibuni katika wilaya ya Kamwenge ya magharibi nchi hiyo.
Msemaji wa Jeshi la Uganda, Kanali Deo Akiiki ametangaza habari hiyo na kumtaja kiongozi huyo wa waasi kwa jina la Musa Kamusi. Hayo yamo kwenye taarifa ya jana Jumatano ya Kanali Akiiki.
Amesema: “Wanajeshi wetu waliokuwa wakiwawinda waasi wa ADF katika Hifadhi ya Kitaifa ya Kibale wamefanikiwa kumuua mmoja wa viongozi wa ADF ambaye amekuwa akiwahangaisha raia huko Kamwenge.”
Ameongeza kuwa, baada ya kumuua kiongozi huyo wa waasi wa ADF, jeshi la UPDF la Uganda limepata pia bunduki moja ya PK na bunduki moja ya AK-47 iliyokuwa na risasi kadhaa. Haya yameripotiwa siku moja baada ya waasi wa ADF kuwashambulia na kuua raia watatu wakiwemo watoto wawili huko Kamwenge.
Wiki iliyopita pia, waasi hao hao waliua watu 10 katika wilaya moja huko Uganda. Jeshi la nchi hiyo limeanza mchakato wa kuajiri askari wa vitengo vya ulinzi vya ndani ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.