Watu wanne nchini Uganda wamekamatwa kwa ‘kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja’, polisi wa nchi hiyo imetangaza siku ya Jumatatu.
Mamlaka iliwakamata watu hao wanne, wakiwemo wanawake wawili, siku ya Jumamosi katika chumba cha masaji katika wilaya ya mashariki ya Buikwe, msemaji wa polisi ameliambia shirika la habari la AFP.
“Operesheni hiyo ya polisi ilifanyika kufuatia taarifa kutoka kwa mwanamke kuashiria kuwa vitendo vya ulawiti vilikuwa vikifanyika katika chumba cha masaji,” amesema Hellen Butoto.
Mwishoni mwa mwezi Mei, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alitia saini sheria inayopinga ushoga ambayo inatoa adhabu kali kwa wale walio na mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja na “wanaoendeleza” ushoga. Uhalifu wa “ushoga uliokithiri” unaadhibiwa kwa kifo, hukumu ambayo, hata hivyo, haijatumika kwa miaka mingi nchini Uganda.
Sheria hii imezua hasira kutoka kwa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kutetea haki za binadamu na nchi nyingi za Magharibi. Mwanzoni mwa mwezi Agosti, Benki ya Dunia ilitangaza kwamba haitafadhili tena miradi mipya nchini Uganda kufuatia kupitishwa kwa sheria hii, ikizingatiwa kuwa nakala hii “inakwenda kinyume na maadili ya Benki ya Dunia”.
Rais wa Marekani Joe Biden aliitaja sheria hiyo “ukiukaji wa kutisha” wa haki za binadamu na kutishia kusitisha misaada na uwekezaji nchini Uganda, huku mkuu wa diplomasia ya Ulaya Josep Borrell akiiona kama sheria hiyo ni “kinyume na haki za binadamu”.