Uganda imesema kuwa imefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa Ebola, ambao ulithibitishwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo mwezi Januari.
Jumla ya wagonjwa nane wa Ebola walithibitika kuruhusiwa kutoka hospitalini siku ya Jumanne, baada ya kuwa wamepona maradhi hayo.
Kulingana na Waziri wa Afya wa Uganda Jane Aceng, licha ya nchi hiyo kuwa imedhibiti ugonjwa huo, mlipuko huo bado haujatoweka kabisa.
Mwishoni mwa mwezi Januari, serikali ya nchi hiyo ilithibitisha mlipuko wa ugonjwa huo, baada ya kifo cha muuguzi mmoja na kisha kufuatiwa na maambukizi mapya nane.
Ugonjwa wa Homa ya Ebola ni ugonjwa wa hatari unaosababishwa na virusi vya ebola.
Ni miongoni mwa magonjwa ya milipuko yajulikanayo kama homa za virusi vinavyo sababisha kutoka damu mwilini.
Ugonjwa huu kwa asili huanzia kwa wanyama kama vile nyani, kima sokwe na popo.