Uingereza na Ireland zimepata msukumo mkubwa katika harakati zao za kuandaa michuano ya Euro 2028 huku Uturuki ikiitaka UEFA kuwasilisha zabuni kwa pamoja kwa ajili ya Euro 2032.
Licha ya hayo, Uturuki haijaondoa azma yake ya kuandaa michuano ya Euro 2028, hivyo imesalia kuwa mpinzani wa ombi la mataifa matano yanayoshirikisha Uingereza, Ireland Kaskazini, Jamhuri ya Ireland, Scotland na Wales.
Uturuki na Italia zimekuwa zikipambana kuwa mwenyeji wa Euro 2032, lakini sasa zinataka kuwasilisha zabuni pamoja huku Uingereza, Ireland Kaskazini, Jamhuri ya Ireland, Scotland na Wales zikiwasilisha ombi la pamoja la Euro 2028.
UEFA ilisema katika taarifa yake: ‘UEFA inathibitisha kwamba imepokea leo ombi kutoka Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) na Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) la kuunganisha zabuni zao binafsi katika ombi moja la pamoja la kuandaa UEFA EURO 2032.
‘UEFA sasa itafanya kazi na FIGC na TFF kuhakikisha kwamba nyaraka zitakazowasilishwa kwa ajili ya zabuni yao ya pamoja zinakidhi matakwa ya zabuni.’