SERIKALI imesema ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 98.8 na unazalisha zaidi ya Megawatt 1,880.
Kutokana na utekelezaji wa mradi huo, imesema inaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za umeme baada ya kukamilisha kuchakata na kuona uwiano wa fedha zilizotumika kwenye ujenzi huo.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema hayo jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano wa kueleza utekelezaji wa kazi mbalimbali kwenye eneo la Bwawa la Mwalimu Nyerere lililoko mikoa ya Pwani na Morogoro.
“Kwa sababu nimesema Bwawa la Nyerere limekamilika, kwa hiyo kiu kubwa ya watanzania wengi wangependa bei ya umeme ishuke kesho, watanzania subirini kidogo, tumetumia fedha hapa, wataalam wetu watachakata, tutaendelea kuangalia uwiano kwa kuwa bado tunazalisha kwenye vyanzo vingine.
“Lakini mkumbuke fedha hizi tumezichomoa na kusimamisha mambo mengine, ni lazima twende ‘tunajibalansi’ lakini tutafika hatua ambazo tutapunguza gharama za umeme, itakapofika tutawajulisha,” alisema.
Msigwa ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema Tanzania ni moja ya nchi zenye gharama za chini za umeme barani Afrika zinazochangia kupatikana kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi kwa kuwa wanapenda kuwekeza katika sehemu ambazo watapata faida.