Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) Alhamisi ilitoa taarifa ikisema, Ujumbe wa ECOWAS wa Waangalizi wa Uchaguzi uliwasili Liberia mapema wiki hii ili kusimamia uchaguzi wa rais na wabunge utakaofanyika wiki ijayo nchini humo.
Taarifa hiyo ilisema kiongozi wa ujumbe huo wa ECOWAS Bw. Attahiru Jega na timu yake watafanya mkutano wa kazi na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tume ya uchaguzi ya taifa, serikali, asasi za kijamii, vyombo vya habari, idara za usalama, pamoja na vyama vya kisiasa na wagombea.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wapiga kura 2,471,617 kati ya watu milioni 5.4 wa Liberia watapiga kura tarehe 10 Oktoba ili kuchagua rais mpya, maseneta 15 na wabunge 73 wa baraza la wawakilishi.