Ujumbe wa maofisa wa polisi kutoka nchini Kenya hapo jana umewasili nchini Haiti baada ya kuondoka katika uwanja wa ndege wa jiji kuu la Port-au-Prince, ukielekea katika ubalozi wa Marekani nchini humo.
Maofisa hao wa polisi kutoka nchini Kenya wakiongozwa na naibu inspekta jenerali wa polisi Noor Gabow, wako katika misheni ya kuwsaidia polisi wa Haiti katika kukabiliana na magenge ambayo yamehangaisha nchi hiyo kwa muda sasa.
Kenya ilikuwa imejitolea kuongoza ujumbe wa kimataifa ili kusaidia idara ya polisi ya Haiti ambayo ina takriban pôlisi elfu 10, ambao wanawahudumia zaidi ya raia milioni 11.
Mwishoni mwa juma lililopita, maofisa wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, walishtumu kile walichokiita ukatili wa kupindukia wa magenge nchini humo, ambayo yanadhibiti karibu asilimia 80 ya jiji kuu na kusababisha maelfu kukimbia vitongoji kadhaa vya mji huo.
Tangu Januari 1 hadi Agosti 15, zaidi ya watu 2,400 wameripotiwa kuuawa nchini Haiti, zaidi ya 950 wakitekwa nyara na wengine 902 wakijeruhiwa, haya ni kwa mujibu wa msemaji wa haki za binadamu wa umoja huo Ravina Shamdasani.