Viongozi mbalimbali kutoka Ulaya na Kanada walitembelea mji mkuu wa Ukraine siku ya Jumatatu kuadhimisha mwaka wa tatu wa vita vya nchi hiyo na Urusi katika onyesho la wazi la kuunga mkono Kyiv huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu kujitolea kwa utawala wa Trump kuisaidia kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Baadhi ya waungaji mkono muhimu wa Ukraine, akiwemo Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, walikuwa miongoni mwa wageni waliolakiwa katika kituo cha treni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha na mkuu wa wafanyikazi wa rais, Andrii Yermak.
Katika chapisho kwenye X, von der Leyen aliandika kwamba Ulaya ilikuwa Kyiv “kwa sababu Ukraine iko Ulaya.”
“Katika mapambano haya ya kuishi, sio hatima ya Ukraine pekee ambayo iko hatarini. Ni hatima ya Uropa, “aliandika.
Maafisa wa Ukraine na Ulaya wamekerwa na mtazamo wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin na maneno yake magumu kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy wiki iliopita kumuita dikteta.