Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imethibitisha siku ya Alhamisi hii, Septemba 12, kwamba wafanyakazi wake watatu wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa nchini Ukraine katika shambulio ambalo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelihusisha jeshi la Urusi.
Vifo vya watu hao watatu vimekuja siku chache kabla ya mkuu wa shirika hilo, Mirjana Spoljaric, kufanya ziara iliyopangwa kwa muda mrefu huko Moscow, ikiwa ni pamoja na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov. Anatarajiwa huko mwanzoni mwa wiki ijayo.
Shambulio hilo liligonga “magari ya ujumbe wa kibinadamu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu” katika eneo la Donetsk, ametangaza Volodymyr Zelensky, akilaani “uhalifu mpya wa kivita”. “Kwa bahati mbaya, watu watatu wameuawa katika shambulio hilo la Urusi” na wengine wawili wamejeruhiwa, ameongeza rais wa Ukraine kwenye Telegram.
“Ninalaani vikali mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa shirika la Msalaba Mwekundu. Haikubaliki kwamba milipuko ya mabomu inaweza kugonga eneo la usambazaji wa misaada,” amesema Mkuu wa ICRC Mirjana Spoljaric.