Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipotembelea Taasisi ya Kairuki iliyopo Bunju A Jijini Dar es salaam ambayo inatoa huduma ya upandikizaji mimba kwa lengo la kuona huduma zinazotolewa kituoni hapo.
Waziri Ummy amesema tatizo la ugumba bado ni kubwa nchini lakini mpaka sasa hakuna takwimu rasmi za kitaifa ila ulifanyika utafiti mdogo ambao unaonesha 30% ya watu wana tatizo la ugumba huku Duniani inakadiriwa kuwa katika kila mahusiano ya wenza wanne, mmoja kati yao anakua na tatizo la kupata Watoto.
“Tatizo la kutopata Watoto lipo pande zote mbili, upande wa Wanaume na Wanawake lakini Jamii yetu inachukulia Familia isipopata Mtoto basi Mwanamke ndiyo anaonekana mwenye tatizo, naamini uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa fikra potofu”
Kituo cha upandikizaji mimba cha Kairuki kinatoa huduma hiyo kwa gharama ya kuanzia Shilingi milioni 13 hadi milioni 17 kutegemea na aina ya huduma inayohitajika, hata hivyo Waziri Ummy amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kuweka nusu ya gharama hizo katika vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote ili kuweza kuwapunguzia wananchi gharama za kupata huduma hiyo.