Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amethibitisha kuwa ushirikiano endelevu baina ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Umoja wa Mataifa (UN) ni wa muhimu katika kutekeleza ajenda mbalimbali za pamoja kwa manufaa ya dunia.
Dkt. Tulia alitoa kauli hiyo tarehe 23 Septemba, 2024, alipokuwa akiwasilisha hotuba kwa niaba ya IPU katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliojadili mustakabali wa dunia kwa siku zijazo (Summit of the Future), uliofanyika katika Ofisi za UN jijini New York, Marekani.
Akiwasilisha hotuba yake, Dkt. Tulia alieleza kuwa kwa zaidi ya robo karne tangu kuanzishwa kwa Azimio la Milenia, ushirikiano kati ya IPU na UN umeonesha mafanikio makubwa, ambapo kwa kila mwaka wameweza kufikia malengo ya kuiwezesha UN kuwa Taasisi inayowajibika, yenye uwazi na inayotekeleza maazimio yake ipasavyo.
Aidha, alibainisha kuwa nafasi ya Mabunge imeainishwa wazi katika lengo namba 55 la Azimio la Pact of the Future, ambalo linaelekeza kuimarisha ushirikiano kati ya Mabunge na Umoja wa Mataifa.
Akisisitiza umuhimu wa wajibu wa Mabunge, Dkt. Tulia alinukuu maneno ya Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyesema “Inawezekana, tekeleza wajibu wako” akiongeza kuwa Umoja wa Mabunge Duniani unatimiza wajibu wake kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa imara kwa kupitia Mabunge.
“Dunia inahitaji mabadiliko na sehemu pekee ya kufanya mabadiliko hayo ni ndani ya Umoja wa Mataifa, na wakati wa kufanya hivyo ni sasa,” alisisitiza Dkt. Tulia.