Shirika moja la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya misaada ya kibinadamu limesema kuwa, maelfu ya watu wamekwama katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa inayonyesha katika jimbo la Jubbaland nchini Somalia.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetoa taarifa hiyo na kuongeza kuwa, mvua kubwa iliyonyesha mwezi uliopita imeongeza kiwango cha maji katika mto Juba na kusababisha mafuriko katika maeneo ya mito ya jimbo hilo.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: “Watu 2,400 wamenaswa katika maeneo yaliyofurika na kuzingirwa na maji kila upande kwenye wilaya ya Luuq.”
Juhudi za mamlaka za serikali na na washirika wa uokoaji zinaendelea kuwaondoa watu waliokwama katika maeneo hayo.
Baadhi ya mashirika ya hahbari yameripoti kuwa, takriban watu 14 wamekufa na 47,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mafuriko yaliyotokea nchini Somalia tangu mwezi uliopita.
Habari hiyo imethibitishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Haki za Binadamu (OCHA) ambalo limesema kuwa, mbali na zaidi ya watu 47,000 kukimbia makazi yao, watu wengine wasiopungua 2,400 wameshindwa kuondoka kwenye maeneo yao kutokana na kuzingirwa na maji kila upande huko katika wilaya ya Luuq.