Umoja wa Mataifa umezitaka mamlaka nchini Iran, kuachana na sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni ambayo inatoa adhabu ya juu kwa wanawake ambao watakiuka uvaaji wa mavazi ya kiislamu, UN ikisema sheria hiyo ni kandamizi.
Katika taarifa yake, ofisi ya haki za binadamu imesema inaguswa na sheria hiyo, iliyosema inawalenga wanawake ambao hawatavalia hijabu, ambapo adhabu ya juu ni kifungo cha miaka 10 jela.
Msemaji wa tume hiyo, Ravina Shamdasani, amewaambia waandishi wa habari kuwa, sheria hiyo ni gandamizi dhidi ya wanawake na wasichana ambao watabainika kukaidi.
Mbali na kifungo gerezani, wanawake watakaokutwa na hatia pia watatozwa faini na kuzuiwa kusafiri nje ya nchi hiyo.
Uamuzi wa Iran umekuja baada ya mwaka uliopita kushuhudiwa maandamano makubwa ya wanawake yaliyochochewa na kifo cha Mahsa Amini, ambaye alipoteza amiahs aakiwa kizuizini baada ya kukamatwa amekiuka sheria ya vazi la hijabu.
Wiki hii mke wa rais wa Iran alitetea sheria iliyopitishwa wiki hii iliyoundwa kutoa hukumu kali zaidi kwa wanawake ambao hawavai hijab hadharani, akilinganisha sheria hizo na “mavazi kila mahali” katika mahojiano na kituo cha habari cha ABC.