Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric, jana amesema, utafiti uliofanywa na Umoja huo umeonesha kuwa idadi ya watu watakaokabiliwa na ukosefu wa chakula katika eneo la Afrika ya Kati na Magharibi mwaka ujao inakadiriwa kuongezeka na kufikia milioni 49.5.
Akinukuu ripoti za utafiti uliofanywa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, Shirika la Kuhudumia Watoto, na Shirika la Chakula na Kilimo, Dujarric amesema, mashirika hayo yamezitaka serikali za nchi mbalimbali na washirika wa kifedha ziweke kipaumbele katika miradi inayoimarisha mifumo ya chakula na maisha inayostahimili hali ya hewa, na kuwekeza katika mifumo ya ulinzi wa jamii.
“Pia walipendekeza maendeleo kwa wakati na utekelezaji wa mipango ya dharura ambayo inashughulikia mahitaji ya haraka ya chakula na lishe kwa watu wanaokumbwa na shida na viwango vya dharura vya uhaba wa chakula,” msemaji huyo alisema.
Uchambuzi ulionyesha hali ya njaa inatia wasiwasi hasa katika nchi za pwani, ambapo idadi ya wanawake, wanaume, na watoto wanaokabiliwa na njaa kali inatarajiwa kufikia milioni 6.2, ongezeko la asilimia 16 zaidi ya mwaka huu, mashirika matatu yaliripoti.