Hatimaye baada ya kusota kwa muda mrefu golikipa wa klabu ya Simba kutoka nchini Ghana Yaw Berko wa Simba amepata kibali cha kufanya kazi nchini, lakini kwa sasa atakuwa chaguo la pili katika kikosi cha kocha Zdravko Logarusic.
Golikipa huyo ambaye alijiunga na Simba mwishoni mwa mwaka jana, hakuweza kuruhusiwa kuitumikia Simba katika ligi kuu kwa sababu hakuwa na na kibali cha kufanya kazi ndani ya mipaka ya Tanzania, lakini hatimaye wiki iliyopita alipata kibali hicho.
Alipozungumza na gazeti la Mwanaspoti, kocha wa magolikipa wa Simba, Idd Pazi amesema kwamba Berko amepata kibali lakini itabidi afanye kazi kubwa kupigania nafasi ya kwanza kukaa kwenye milingoti mitatu ya Simba.
“Pamoja na Berko mambo yake kuwa sawa, hawezi kuwa namba moja kwani Mapunda ndiye chaguo la kwanza. Nafasi ya Berko kucheza namba moja itakuja endapo Mapunda atafanya vibaya.
“Hiyo ndiyo falsafa ya kocha (Logarusic), anasisitiza huwezi kumtoa mchezaji katika nafasi yake wakati hajafanya vibaya. Tusubiri kuona kama Mapunda atafanya makosa ya kizembe uwanjani,” alisema Pazi.
Hata hivyo nafasi ya Berko inaweza kutazamwa katika mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga baada ya Mapunda kuruhusu bao ‘jepesi’ dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatano iliyopita.
Bao hilo lilifungwa dakika ya nane baada ya Mapunda kushindwa kuudaka mpira wa krosi uliopigwa na Mussa Mgosi kutoka wingi ya kulia.
Mapunda aliutumbukiza mpira wavuni akiwa katika harakati za kuokoa. Ingawa benchi la ufundi limemtetea na kufafanua kuwa kosa lilikuwa la beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.