Katika taarifa, UNICEF imetoa wito wa ufadhili zaidi kusaidia sio tu kulinda watoto zaidi na jamii zinazohitaji lakini kubuni mifumo thabiti zaidi ya kulinda watoto katika siku zijazo.
UNICEF imese hatari ni kubwa zaidi kwa watoto na kuonya kwamba mahitaji katika jamii zilizoathirika mashariki na kusini mwa Afrika yanaongezeka.
Shirika hilo limeomba msaada wa dharura wa dola milioni 171 kujibu mahitaji yanayoongezeka ya watu milioni 28, wakiwemo watoto na familia zao katika eneo lililoathiriwa na kipindupindu.
Fedha hizo zitatengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma za maji ya kuokoa maisha, usafi wa mazingira na usafi, afya, lishe, ulinzi wa mtoto na huduma za elimu kwa wanawake na watoto walioathirika na mlipuko huo.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema wakati wafadhili tayari wamechangia dola milioni 18.3 kusaidia kukabiliana na kipindupindu, pengo la ufadhili wa kikanda linahitaji kuzibwa haraka ili kukabiliana na hali iliyoibuka.
Mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu kuwahi kutokea katika ukanda huo kwa miaka mingi umeripotiwa katika nchi 11 zikiwemo Burundi, Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji, Somalia, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Takriban kesi 67,822 zimerekodiwa na vilevile vifo vinavyokadiriwa 1,788, kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya UNICEF.
Huko Msumbiji Mkurugenzi wa afya katika jimbo la Zambezia, Blayton Caetano ameiambia radio ya serikali ya Msumbiji kwamba inajiandaa na zoezi la kutoa chanjo dhidi ya kipindupindu na litachukua muda wa wiki mbili.
Shughuli hiyo ikilengw kupunguza maambukizi ya kipindupindu ambapo idadi yake ilikuwa juu mno baada ya kimbunga cha kihistoria.
Uharibifu mkubwa ulitokea Quelimane kutokana na kimbunga Freddy kilichoua watu 19 na kupelekea watu 50,000 kupoteza Makazi.
Msumbiji imesema Jumanne kwamba imepokea dozi milioni 1.7 za chanjo dhidi ya kipindupindu. Chanjo hiyo imetolewa na UNICEF.