Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka taasisi ya tiba ya magonjwa ya mifupa na ubongo muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na madaktari na wataalamu wenzao wa hospitali ya rufaa ya kanda chato (czrh) kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo (Brain Tumor) kwa mtoto wa miaka tisa (9) aliyekuwa na uvimbe upande wa kulia na kushoto wa ubongo tatizo lililopelekea mtoto kupoteza ufahamu pamoja na kupooza kwa miguu na mikono.
Upasuaji huu umefanyika kupitia kambi inayoendelea ya matibabu ya magonjwa ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu iliyozinduliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Bw. Mohamed Gombati katika hospitali ya rufaa ya kanda chato.
Akizungumza mara baada ya upasuaji, Dkt. Alpha Kinghomella, Daktari Bingwa mbobezi wa ubongo kutoka MOI amesema wamefanya upasuaji kwa mtoto wa miaka tisa ambaye tulimfanyia uchunguzi na kugundua ana uvimbe katika pande zote mbili za ubongo , yaani kulia na kushoto mwa ubongo, hali iliyompelekea kushindwa kujitambua lakini pia mikono na miguu yote haikuwa ikifanya kazi.
Dkt. Kinghomella ameongeza na kusema wamefanikiwa kuuondoa uvimbe upande mmoja ambao tumechukua sampuli kwa ajili ya vipimo zaidi huku tukingoja majibu ambayo yatasaidia kuendelea kumpatia matibabu. Kwa sasa mtoto anaendelea vizuri na ameanza kujitambua na kuweza kuongea, na kwa kipindi chote cha matibabu yake atakuwa chini ya uangalizi wa madaktari wetu.
Hadi sasa, zaidi ya wananchi 200 wamepata matibabu na kati yao, wagonjwa 7 tayari wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo, magoti na pingili za mgongo.
Zoezi hili la matibabu kibingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa wa mifupa, ubongo, mgongo pamoja na mishipa ya fahamu bado yanaendelea kutolewa na Madaktari bingwa wa MOI katika hospitali ya rufaa ya kanda chato zoezi ambalo ni endelevu.