Upelelezi wa kesi ya usafirishaji wa dawa za kulevya Kilogramu 34.89 aina ya Heroin, inayomkabili aliyekuwa Kocha wa Makipa wa klabu ya Simba, Muharami Sultan na wenzake umekamilika.
Wakili wa Serikali, Carolina Matemu amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mario kwamba tayari upelelezi wa shauri umekamilika, wamepeleka taarifa Mahakama Kuu hivyo wanasubiri irudi ili waweze kuwasomea maelezo ya mashahidi washitakiwa hao.
Kutokana na hali hiyo, aliiambia mahakama kwamba ipange tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo.
Hakimu amekubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 16, 2023.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sports Academy kilichopo Tuangoma Kigamboni , kinachojihusisha na ukuzaji wa vipaji kimichezo Kambi Seif.
Wengine ni Maulid Zungu, maarufu kama Mbonde, Said Abeid fundi selemala, John Andrew maarufu kama Chipanda mfanyakazi wa kituo cha Cambiasso na Sara Joseph.
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 27 mwaka huu, Kivule , Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 27.10.
Katika shitaka la pili ilidaiwa kwamba, Novemba 4 mwaka huu eneo la Kamegele Mkuranga, Pwani kwa pamoja walikutwa wakisafirisha kilogramu 7.79 za dawa za kulevya aina ya Heroin.