Chama kikongwe cha upinzani nchini Msumbiji, Renamo, sasa kinataka matokeo ya uchaguzi yaliyokipa ushindi chama tawala Frelimo yabatilishwe, wakati huu kinara wa upinzani nchini humo akiitisha maandamano zaidi ya raia.
Renamo kilikuwa chama kikuu cha upinzani hadi baada ya uchaguzi wa Oktoba 9 ambapo chama kingine cha Podemos kinachoongozwa na Venancio Mondlane ilikipiku, kiongozi wake akisema uchaguzi ulikuwa na dosari na kuitisha maandamano.
Akizungumza mjini Maputo, kiongozi wa Renamo, Ossufo Momade, amesema wanataka matokeo ya uchaguzi wa Octoba 9 yabatilishwe na kuitishwa kwa uchaguzi mpya ambao utaaminika.
Tume ya uchaguzi ilikitangaza chama tawala Frelimo kushinda uchaguzi huo kwa asilimia 71 ya kura zote, kikifuatiwa na Podemos kilichopata asilimia 20 na Renamo kiliambulia asilimia 6 pekee.
Haya yanajiri wakati huu kwa majuma kadhaa kinara wa upinzani Venancio Mondlane, aliyeko uhamishoni Afrika Kusini, ameitisha maandamano ya kila wiki kupinga ushindi wa chama tawala, maandamano yaliyotawaliwa na vurugu kati ya polisi na raia.