Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jonsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameiasa jamii kuona umuhimu wa malezi bora kwa watoto ndani ya familia kama chanzo cha jamii.
Ametoa wosia huo Aprili 18, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia hapo Mei 15, 2024.
Waziri Dkt. Gwajima amesema, Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kutathmini nafasi ya familia katika ustawi na maendeleo yao na mchango wao kwa taifa ambapo mwaka huu 2024 maadhimisho yatafanyika kimikoa kwa kugusa ngazi ya jamii yaani Vijiji, Mitaa na Kata.
Akielezea hali ya sasa kwa mujibu wa utafiti wa hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022, Dkt. Gwajima amebainisha
mifarakano na migogoro katika familia imesababisha malezi duni na uangalizi hafifu wa watoto hususan watoto wa kike iliyopelekea watoto hao kuanza ngono katika umri mdogo jambo ambalo limesababisha mimba za utotoni kuendelea kuwepo kwa kiwango kikubwa.
“Asilimia 27 ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, 12% kati yao walifanyiwa ukatili wa kingono. Vilevile, asilimia 13 ya wanawake waliowahi kuwa na mume katika kipindi cha miezi 12 kabla ya utafiti huo walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono na kihisia.” amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima