Jeshi la Urusi lilisema Jumanne kwamba liliharibu ndege 144 za anga za Ukraine zilizorushwa katika mashambulio ya usiku kulenga maeneo ya magharibi mwa Urusi.
Vikosi vya ulinzi wa anga vilidungua ndege 20 zisizo na rubani katika mkoa wa Moscow, ambapo Gavana Andrey Vorobyov alisema ndege zisizo na rubani ziliharibu majengo ya ghorofa na nyumba huko Lyubertsy na Ramenskoye. Shambulizi hilo liliua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine watatu, Vorobyov alisema kwenye Telegram.
Vizuizi vingi zaidi vilifanyika katika eneo la Bryansk kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine, lakini maafisa waliripoti kuwa hakuna uharibifu au majeruhi baada ya ndege hizo 72 kudunguliwa.
Ulinzi wa anga wa Urusi pia ulishusha ndege zisizo na rubani za Kiukreni kwenye maeneo ya Kursk, Tula, Belgorod, Kaluga, Voronezh, Lipetsk na Oryol. Magavana katika sehemu nyingi za maeneo hayo walisema kwenye Telegram hakukuwa na ripoti za majeruhi.
Mashambulizi ya hivi punde ya Urusi dhidi ya Ukraine ni pamoja na kutumia ndege zisizo na rubani kulenga eneo la Kyiv, ambalo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara mwezi huu.
Serhiy Popko, mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kyiv, alisema kwenye Telegram kwamba arifa za anga zilisikika kwa saa mbili Jumanne, lakini kwamba ulinzi wa anga wa Ukraine ulitungua ndege zote zisizo na rubani za Urusi zilizoelekezwa mji mkuu.
Kikosi cha anga cha Ukraine kilisema Jumanne kiliangusha ndege 38 kati ya 46 zilizotumiwa na Urusi katika mashambulizi ya usiku.