Mahakama ya Moscow siku ya Ijumaa ilianza kusikiliza kesi ya mwanamume Mmarekani mwenye umri wa miaka 72 anayetuhumiwa kupigana kama mamluki nchini Ukraine, mashirika ya habari ya Urusi yaliripoti.
Mahakama ya Jiji la Moscow inasikiliza kesi ya jinai dhidi ya Mmarekani huyo “kuhusika kama mamluki katika mzozo wa kijeshi upande wa Ukraine,” shirika la habari la RIA Novosti lilisema.
Ilimtaja mwanamume huyo kuwa ni Stefan Hubbard lakini ikasema jina lake linaweza kuandikwa tofauti, huku machapisho kwenye mitandao ya kijamii yakipendekeza jina hilo linaweza kuwa Stephen Hubbard.
“Tunafahamu taarifa za kukamatwa kwa raia wa Marekani. Kwa sababu ya vikwazo vya faragha hatuwezi kutoa maoni yoyote zaidi, “ubalozi wa Marekani huko Moscow ulisema katika taarifa.
Mstaafu huyo kutoka Michigan alihamia Ukraine mnamo 2014, RIA Novosti alisema. Ripoti hazikuweka wazi ni lini au jinsi gani Hubbard aliwasili Moscow.
Katika kesi hiyo katika mahakama ya juu zaidi ya jiji la Moscow, hakimu alikubali ombi la mwendesha-mashtaka la kumzuilia Hubbard kwa miezi sita kwa sababu angeweza kujaribu kutoroka, na kumweka rumande hadi Machi 26, 2025.
Kesi inayofuata ilipangwa Alhamisi ijayo.