Urusi imechukua hatua kali kwa kufukuza Wanadiplomasia sita wa Uingereza walioko Moscow, ikiwatuhumu kwa vitendo vya “ujasusi na uharibifu,” kulingana na taarifa iliyotolewa na huduma ya usalama ya FSB ya Urusi.
FSB imedai kuwa ina nyaraka zinazoonyesha idara ndani ya Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza mjini London ilihusika na juhudi za kuongeza mvutano wa kisiasa na kijeshi dhidi ya Urusi, na kuhakikisha kushindwa kwa Urusi katika mzozo wake na Ukraine.
Aidha Kwa mujibu wa FSB, “Matukio yaliyobainishwa yanatoa msingi wa kuzingatia kuwa vitendo vya Wanadiplomasia wa Uingereza waliotumwa Moscow vinahatarisha usalama wa Shirikisho la Urusi”, hivyo kwa misingi ya ushahidi uliotolewa na FSB, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imeamua kufuta vibali vya Wanadiplomasia hawa sita wa ubalozi wa Uingereza.
Runinga ya Serikali ya Urusi ilionyesha picha za Wanadiplomasia hao hadharani, na mwakilishi wa FSB alieleza kupitia kituo cha televisheni cha Rossiya-24 kuwa, “Waingereza hawakuchukua tahadhari zetu juu ya haja ya kuacha vitendo vya kijasusi ndani ya Urusi, kwa hivyo tumeamua kuwafukuza hawa sita kwa kuanzia.”
Aidha FSB imeonya kwamba Wanadiplomasia wengine wa Uingereza wanaweza kufukuzwa ikiwa wataendelea na shughuli zinazofanana.
Hatua hii ni sehemu ya mvutano unaoongezeka kati ya Urusi na Uingereza, huku FSB ikisisitiza umuhimu wa kudumisha usalama wa ndani dhidi ya vitisho vya kijasusi na uharibifu kutoka mataifa ya kigeni.