Shirika la misaada na maendeleo ya kimataifa la Marekani (USAID), na mpango wa chakula duniani (WFP) Jumatano yametangaza kwamba yanasimamisha msaada wa chakula kwa mkoa ulio athirika na vita wa Tigray baada shehena ya msaada kupelekwa katika masoko ya kawaida.
Samanta Power ambaye ni mkuu wa USAID, ambalo ni shirika kuu la misaada ya kimataifa la serekali ya Marekani, amesema kwamba wameamua kufanya uamuzi mgumu wa kusimamisha msaada wa chakula wa USAID mkoani Tigray mpaka watakapo toa taarifa zaidi.
Shirika hilo hivi karibuni lilianzisha msaada mwingine wa chakula uliokuwa na dhamirra ya kupelekwa kwa watu wa Tigray ambao wanakabiliwa na hali ya ukame lakini ulihamishwa na kuuzwa kwenye masoko ya kawaida amesema Samantha Power katika taarifa yake.
WFP pia imesema imesimamisha usambazaji wa chakula mkoani Tigray baada kutambua tatizo la vyakula kupelekwa kwenye kusiko stahili.
Uamuzi huo unakuja kutokana na ugunduzi wa USAID kwamba kiasi kikubwa cha chakula cha msaada kwa watu “walioteseka katika mazingira kama ya njaa kilielekezwa kinyume na kuuzwa katika soko la ndani.” Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani lilipeleka suala hilo kwa mkaguzi wake mkuu wa ndani, ambaye ameanza uchunguzi.
Serikali ya Marekani imeibua wasiwasi na serikali ya shirikisho ya Ethiopia na Utawala wa Muda wa Mkoa wa Tigray, ambao wote walionyesha nia ya kufanya kazi na USAID ili kuwatambua waliohusika na kuwawajibisha, kulingana na taarifa ya Power.
“USAID iko tayari kuanzisha tena usaidizi wa chakula uliositishwa pale tu hatua kali za uangalizi zitakapowekwa na tuna imani kuwa msaada utawafikia walengwa walio katika hatari,” alisema Jumatano.
Tangazo la USAID linakuja baada ya Associated Press kuripoti wiki hii kwamba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limesitisha programu zake za msaada wa chakula huko Tigray huku likifanya uchunguzi wa ndani kuhusu wizi wa chakula. Majibu mengi ya WFP huko Tigray yanafadhiliwa na USAID.