Mkazi wa Buguruni, Thomas Mgoli (37) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi ikiwemo kujifanya Afisa Usalama wa Taifa anayetaka kumsaidia aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Magoli amesomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina.
Katika kesi hiyo namba
namba 98 ya mwaka 2019, kosa la kwanza la kujifanya Afisa wa Serikali alilitenda katika tarehe tofauti kati at Desemba 1, 2017 na Agosti 2019 katika eneo la Mahabusu ya Keko ambapo alijifanya Mtumishi wa Umma aliyeajiriwa kitengo cha Usalama wa Taifa.
Pia kosa jingine inadaiwa alijipatia Pesa kwa njia ya udanganyifu ambalo amelitenda Agosti 17, 2019 na Agosti 29, 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam ambapo alijipatia Sh.Laki Tatu kutoka kwa Lucy Mgongokesi akijifanya Afisa Usalama anayetaka kusaidia kesi namba 213/2017 ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Jamal Malinzi.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Mhina alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpatia mshitakiwa dhamana, pia haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya Uhujumu Uchumi hivyo mshtakiwa atakwenda rumande.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, ambapo kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4, 2019.