Mke wa aliyekuwa nguli wa mpira wa kikapu Vanessa Bryant, amekubali kulipwa fidia ya $28,850,000 kutokana kesi ya madai aliyoifungulia Kaunti ya Los Angeles nchini Marekani, kutokana picha ambazo maafisa wa polisi wa Kanuti hiyo walizipiga na kuzisambaza baada ya ajali ya helikopta iliyomuua mume wake Kobe Bryant pamoja na binti yake Gianna mnamo Januari 2020, kulingana na mawakili wa kaunti. Mshtaki mwenza Chris Chester, ambaye mke wake na binti yake pia waliuawa kwenye ajali hiyo, wamekubali kulipwa $19,950,000.
Kutokana na taarifa iliyotolewa na wakili aliyesimamia kesi hiyo, alisema kuwa hii itakuwa kilele chenye mafanikio kwa Vanessa Bryant ambae alipigania haki ya mume wake, binti yake pamoja na wote waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo mbaya, huku walioshiriki kwenye vitendo hivyo visivyofaa wakiwajibishwa. Mawakili wa Kaunti ya LA walisema wanatumaini familia za Bryant na Chester zitaweza kupona kutokana na changamoto walizozipitia.
“Tunaamini kwamba suluhu iliyoidhinishwa na Bodi katika kesi ya Bryant ni ya haki na ya kuridhisha. Suluhu hio ya $28,850,000 linajumuisha uamuzi uliotolewa na mahakama ya shirikisho mnamo Agosti 2022 na kusuluhisha masuala yote ambayo bado hayajashughulikiwa yanayohusiana na madai ya kisheria yaliyosalia katika mahakama ya serikali, madai yoyote yaliyosalia kuhusiana na watoto wa Bryant na gharama nyinginezo, huku kila upande ukiwajibika kwa ada za mawakili wake,” Mira Hashmall, wakili mkuu wa kesi ya LA County katika kesi ya Bryant-Chester, alisema katika taarifa.
Kobe Bryant na binti yake Gianna, walikuwa wakielekea kwenye mechi ya mpira wa kikapu katika chuo chake cha michezo kiitwacho ‘Mamba Sports’ huko Thousand Oaks nchini Marekani pamoja na wengine waliokuwa wakisafiri nao mnamo Januari 26, 2020 wakati helikopta waliyokuwa wakisafiria ilipoanguka huko jijini Calabasas nchini Marekani. Watu wote tisa waliokuwa kwenye helicopter hiyo waliuawa.
Vanessa Bryant aliwasilisha kesi mahakamani miezi kadhaa baada ya ajali hiyo dhidi ya Kaunti ya Los Angeles, akidai kuwa maafisa wa Kaunti ya Los Angeles walichukua picha za mabaki ya binadamu waliopoteza maisha kwenye eneo la tukio kama “ukumbusho” na kuzisambaza huku akidai kuwa alipitia changamoto za kihisia na kuweweseka usiku na kuishtaki taasisi hiyo kwa uzembe na uvamizi wa haki za faragha. Mnamo Agosti 2022, mahakama ilimzawadia Vanessa Bryant dola milioni 16 kama fidia kutokana na kesi ya faragha dhidi ya Kaunti ya Los Angeles