Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mkoani Iringa kimeadhimisha miaka 30 ya VETA na miaka 50 ya ufundi stadi huku ikijivunia muitikio wa wananchi kujiunga na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na chuo hicho.
Maadhimisho hayo ya siku mbili yamehitimishwa katika Chuo cha elimu ya mafunzo ya ufundi stadi Mkoani Iringa ambapo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha mapinduzi ambapo Mkuu wa Chuo hicho Pasiens Nyoni amewataka wananchi kupata mafunzo rasmi kupitia VETA ili wapate vyeti vitakavyowafanya kutambulika maeneo mbalimbali katika fani zao kulingana na ujuzi waliosomea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa VETA kanda ya Nyanda za juu Kusini Suzan Magani ameeleza kuwa ndani ya miaka 30, VETA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kuna ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi stadi kutokana na kuongezeka kwa vyuo sita kwa kuwa hapo awali kulikuwa na vyuo viwili pekee (Iringa na Songea) hivyo kwa sasa kufanya kuwa na idadi ya vyuo nane kwenye Mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini.
Nao baadhi ya wanafunzi wanaopata mafunzo mbalimbali chuoni hapo wameeleza furaha yao kwa uwepo wa VETA kwani mafunzo wanayopata yatawasaidia kujiajiri na kuendesha maisha yao baada ya kuhitimu.
Maadhimisho ya VETA na ufundi stadi kitaifa yanatarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere kuanzia Tarehe 18 hadi 21 Mwezi Machi mwaka huu.
Hatahivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi amewataka madereva wa vyombo vya moto Iringa kuwa na utaratibu wa kuendelea kupata mafunzo ya vyombo hivyo ili kuongeza umahiri wa fani hiyo kulingana na daraja la leseni husika ili kuendana na mabadiliko ya sheria za barabarani zinazojitokeza.
Katika hatua nyingine Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Salim Abri ambaye ameshiriki darasa la mafunzo ya udereva, ameweka wazi kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu yanasaidia zaidi kwa madereva waliopata mafunzo miaka mingi iliyopita hivyo kusaidia kuendana na kasi ya ongezeko la watumiaji wa vyombo vya moto.
VETA Mkoa wa Iringa leo imehitimisha maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake na miaka 50 ya ufundi stadi huku ikijivunia kuongezeka kwa wanafunzi pamoja na ongezeko la vyuo kwenye mikoa iliyopo nyanda za juu Kusini.