Mfanyabiashara Abdullah Hauga mwenye umri wa miaka 73 aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika meli bila kibali leo February 5, 2018 ameachiwa huru baada ya DPP kuondoa mashtaka dhidi yake.
Mbali ya Hauga mshtakiwa mwingine ambaye hakuachiwa huru ni Mkurugenzi wa Meli ya Lucky Shipping, Issa Haji (39). Wakili wa serikali, Salim Msemo amemueleza Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victoria Nongwa kwamba shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya uamuzi kuhusu DPP kuzuia dhamana kwa washtakiwa.
Akisoma uamuzi huo, Hakimu Nongwa amesema alisikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili ambapo pia amesoma uamuzi wa February 2, 2018 wa Mahakama ya Rufaa ambapo imemuondolea DPP mamlaka ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa.
Hakimu Nongwa amesema Mahakama ya Rufaa ndio ya juu nchini, hivyo maamuzi yake lazima yaheshimiwe kwani katika uamuzi wake imebainisha kuwa kuzuia dhamana kwa washtakiwa ni sawa na kuwanyima haki.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Nongwa amesema anatupilia mbali kibali cha DPP kuzuia dhamana kwa washtakiwa na anawapa masharti ya dhamana.
Baada ya kueleza hayo, Wakili Msemo alieleza Mahakama kwamba DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa wa pili ambaye ni Hauga.
Kutokana na hatua hiyo Hakimu Nongwa akamuachia huru Hauga, huku mshtakiwa wa kwanza akirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi imeahirishwa hadi February 18, 2018.
Walivyofikishwa Mahakamani waliopeperusha Bendera ya Tanzania katika meli