Idadi ya vifo kutokana na moto mkubwa uliozuka katika shule ya Hillside Endarasha Primary, kaunti ya Nyeri, Kenya, imeongezeka hadi watu 21 baada ya miili zaidi kupatikana mwishoni mwa wiki.
Miili 19 ilipatikana eneo la tukio, huku Watoto wawili wakifariki Hospitalini kutokana na majeraha waliyopata.
Kwa mujibu wa Daktari wa Serikali, Johansen Oduor, miili hiyo imeungua vibaya kiasi kwamba itakuwa vigumu kwa wazazi kuitambua, Upimaji wa DNA unatarajiwa kuanza leo hii ili kusaidia kutambua miili ya watoto hao, ingawa maafisa wa Serikali wamesema mchakato huo utachukua siku kadhaa.
Moto huo ulitokea usiku wa Alhamisi, ambapo uliteketeza Bweni lililokuwa na Watoto wa kiume 156 wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14, Zaidi ya watoto 100 wamepatikana, lakini watoto 17 bado hawajulikani walipo.
Serikali imewataka waliowasaidia Wanafunzi wakati wa Moto huo kuwarudisha Shuleni ili kusaidia kuwatafuta.
Eneo la tukio limefungwa kwa ajili ya uchunguzi, lakini chanzo cha Moto bado hakijajulikana, Aidha Rais William Ruto ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia Jumatatu leo.
Kwa wakati huo huo, Shirika la Msalaba Mwekundu linaripoti Moto mwingine uliotokea katika Shule ya Wasichana mjini Isiolo, ambapo Wanafunzi watatu wamejeruhiwa.
Moto huo umesababisha uharibifu wa Mabweni kabla ya kudhibitiwa, Serikali imehimiza Shule kufuata miongozo ya usalama katika Mabweni ili kupunguza majanga kama haya.