Waziri wa Nishati, January Makamba leo amewasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake kwamba kwa sasa jumla ya Vijiji vilivyounganishwa na umeme nchini vimefikia 10,127 sawa na 82% ya Vijiji vyote 12,318.
“Kwa kutambua kuwa Sekta ya Nishati ndiyo mhimili muhimu wa maendeleo ya Nchi yetu, muelekeo wa Wizara ni kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawati 1,872.05 za sasa na kufikia Megawati 5,810.22 mwaka 2025/26 ili kukidhi mahitaji ya umeme nchini, utekelezaji wa maono hayo umezingatia umuhimu wa utekelezaji wa miradi ya uzalishaji umeme unaotokana na vyanzo mbalimbali ambapo ushiriki wa Sekta binafsi utazingatiwa”
“Kwakuwa umeme ukishazalishwa lazima usafirishwe na kusambazwa kwa watumiaji, muelekeo wa Wizara ni kuongeza idadi ya njia za kusafirisha umeme kutoka kilomita 6,110.28 za mwaka 2021/22 hadi kufikia kilomita 10,670.95 mwaka 2025/26, kwa upande wa njia za usambazaji umeme, muelekeo ni kufikia kuongeza njia hizi kutoka kilomita 154,567.75 za mwaka 2021/22 hadi kufikia kilomita 226,302.64 mwaka 2025/26.
“Serikali itatilia mkazo matengenezo na utunzaji endelevu wa miundombinu ya umeme, pamoja na kukabiliana na upotevu wa umeme, dhamira yetu ni kuhakikisha kunakuwepo na tija na ufanisi katika umeme unaozalishwa, kusafirishwa, kusambazwa na kutumika”