Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema Jumanne kwamba iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano yatapitishwa na Urusi, “angalau askari 200,000 wa kulinda amani wa Ulaya” watahitaji kuwepo nchini Ukraine kuilinda nchi hiyo ya Ulaya Mashariki dhidi ya mashambulizi yanayoweza kufanywa na Urusi.
Zelenskyy, akizungumza siku moja baada ya Donald Trump kurejea katika kiti cha urais wa Marekani, alisema Ulaya lazima “ijitunze.” Alisema walinda amani 200,000 kutoka nchi za Ulaya watakuwa idadi ya chini zaidi ya walinda amani wanaohitajika, “Vinginevyo, si lolote.”
“Tusisahau, hakuna bahari inayotenganisha nchi za Ulaya na Urusi,” Zelenskyy alisema katika hotuba yake kwenye Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos, Uswizi. Rais wa Ukraine alisema matakwa ya Urusi kwamba Ukraine ipunguze jeshi lake hadi moja ya tano ya ukubwa wa sasa wa 800,000 sio chaguo.
Utetezi bora wa Ukraine wakati wa makubaliano ya kusitisha mapigano, Zelenskyy alisema, itakuwa uanachama wake katika NATO.
Wakati nchi nyingi za Ulaya zinaunga mkono kuingia kwa Ukraine katika muungano huo, Ujerumani na Marekani zinapinga. Hungary na Slovakia, ambazo ni serikali zinazounga mkono Urusi, pia zinapinga Ukraine kuingia katika NATO.