Taasisi, chi mbalimbali na viongozi karibu wote duniani wanalaani mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon. Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Madola zote zinalaani mapinduzi ya hivi punde barani Afrika.
Morocco “inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Gabon,” imesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco, ikisisitiza umuhimu wa kuhifadhi utulivu wa nchi hii ndugu.
Mwishoni mwa mwaka 2018, Ali Bongo alichagua kupumzikia Morocco katika hospitali ya kijeshi ya Rabat baada ya kulazwa hospitalini huko Saudi Arabia kufuatia kiharusi. Mfalme Mohammed wa 6 alimtembelea hospitalini.
Nchini Nigeria, Rais Bola Ahmed Tinubu amesema anawasiliana na wakuu wengine wa nchi za Afrika kuhusu utawala wa kiimla unaoambukiza ambao tumeona ukienea katika bara zima. Madaraka ni ya raia wa Afrika na si ya mtutu wa bunduki, Tinubu amesema kupitia msemaji wake.
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amelaani vikali kile alichokitaja kuwa jaribio la mapinduzi nchini Gabon. Anawahimiza wanasiasa kutumia njia za kisiasa kwa amani.
Nchini Ufaransa, ambaye kutimuliwa mamlakani kwa Bw. Bongo kutaleta pigo zaidi kwa ushawishi wake barani Afrika, serikali imesema inalaani mapinduzi yanayoendelea Gabon na kusisitiza nia yake ya kuona matokeo ya uchaguzi yanaheshimiwa.
Kwa upande wa Umoja wa Ulaya, wanaamini kuwa mapinduzi hayo, yatazidisha ukosefu wa utulivu katika kanda hiyo.
Jumuiya ya Madola ambayo Gabon imejiunga nayo hivi punde, imesema inasikitishwa na hali ya wasiwasi nchini, ikikumbusha nchi hii juu ya majukumu yake katika suala la kuheshimu demokrasia.
Urusi imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali hiyo, huku China ikitoa wito kwa pande zote nchini Gabon kudhamini usalama wa Bongo, “kusuluhisha tofauti kwa njia ya mazungumzo na kurejesha utulivu wa kikatiba haraka iwezekanavyo”.
Hatimaye, Ikulu ya White House “inafuatilia hali kwa karibu sana”. John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa, ametaja mfululizo wa mapinduzi barani Afrika kuwa wa wasiwasi sana. Jeshi linashikilia mamlaka katika nchi za Mali, Guinea, Sudan, Burkina Faso na takriban mwezi mmoja uliopita nchini Niger.