Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza viongozi wa Dini nchini kuendelea kusimamia misingi ya malezi na makuzi ya kwa watoto ili kuhakikisha tunu ya amani iliyopo nchini inalindwa na kuhifadhiwa.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza katika ufungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God (Tanzania) uliofanyika Jijini Dodoma, ambapo amesema Kanisa linatakiwa kulinda amani iliyopo na daima viongozi wa dini wasikubali tofauti za kibinadamu zitumike kuondosha amani ya nchi.
“Kuna watu ni wakandarasi wa uongo na wengine ni mawakala wa uongo; PAG tukawafundishe watu kuwa uongo wa aina hiyo, unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuna watu wangependa tofauti zetu za dini, kabila na mitazamo yetu igeuzwe mtaji wa kisiasa, tusikubali na tuendelee kuwa wamoja na kuilinda tunu ya amani yetu” amesema Dkt. Biteko
Amesema Tanzania ni kama familia inayojengwa na kila mtu wakiwemo viongozi wa Dini na Taifa bora litapatikana kutokana na familia bora huku akikisisitiza umuhimu wa kuzilinda mila nzuri na kujiepusha na tamaduni zinazosababisha mmomonyoko wa maadili ya jamii.
“ Baadhi ya nchi Duniani zimekumbwa na machafuko lakini sisi tuna bahati kuishi kwa amani hatudhuriani kutokana na tofauti zetu na amani tuliyonayo ni tunu, hivyo Kanisa lione umuhimu wa kulinda tunu hii na anayetaka kuvunja amani hiyo tofautianeni naye” amesema na kuongeza kuwa viongozi wa dini wakawambie waumini kwamba jambo la msingi katika familia na taifa ni maendeleo na amani na hivyo wahimize wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu ukifuatiwa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Akizungumza wakati wa akimkaribisha mgeni rasmi, Askofu Mkuu wa PAG(Tanzania) Dkt. Daniel Awet ameiomba Serikali kuendeleza mazingira rafiki kwa Watanzania ili kuimarisha Demokrasia, haki na misingi ya amani iliyodumu kwa miaka mingi.
Aidha, amemwomba Dkt. Biteko afikishe salamu za Kanisa hilo kwa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimweleza kuwa waumini wanatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali anayoingoza na wao kama raia wake wanashirikiana naye kujenga na kulinda amani ya nchi.
Askofu Dkt. Awet pia amewasilisha changamoto ya mgogoro wa kiwanja katika eneo la sabasaba Jijini Dodoma na uvamizi wa kiwanja kingine kinachodaiwa kuvamiwa na wachimbaji wa madini ambapo Dkt. Biteko ameelekeza ufuatiliaji wa changamoto hiyo na yeye apatiwe nakala za Barua husika kwa ajili ya hatua za maamuzi.