Familia ya Mtanzania Nemes Raymond Tarimo (34) ambaye ameripotiwa kufariki wakati akipigana upande wa Jeshi binafsi la Urusi la Wagner Group dhidi ya Ukraine, imesema haifahamu ni nini kimempata Kijana wao hadi kufariki kwakuwa wanachokifahamu wao ni kwamba Nemes alikuwa anasoma Urusi na wameshangaa kuona akiagwa kijeshi.
Video ambayo imesambaa mitandaoni inawaonesha Wapiganaji wanaominika ni kutoka Wagner Group wakimuaga Nemes Tarimo ambapo amepewa pia nishani baada ya kudaiwa kufariki vitani katika shambulio la Bakhmut Mkoa wa Donbas mashariki mwa Ukraine.
Mjomba wa Nemes, Andrew Mwandenuka akiongea nyumbani kwa Familia ya Nemes Dar es salaam leo, amesema Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi umeiambia Familia kuwa mwili wa Nemes utakapofikishwa Tanzania wataelezwa ni nini kimempata Kijana wao.
Jitihada za @ayotv_ kuupata Ubalozi wa Tanzania katika Shirikisho la Urusi ili kupata taarifa za tukio hili hazijafanikiwa huku Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukisema unalifanyia kazi suala hilo.
Yapo madai ambayo hayajathibitishwa yanayodai Nemes alifungwa Jela na baadaye alipewa nafasi ya kutoka jela kwa sharti la kujiunga na Jeshi hilo lakini Familia inasema haina taarifa za kwamba Nemes alifungwa wala kujiunga na Jeshi na inachokifahamu ni kwamba alikuwa Mwanafunzi