Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amevitaka vyombo vya usalama nchini kuwa mstari wa mbele katika kupambana na matumizi na uimgizwaji wa dawa za kulevya nchini.
Mhe. Abdullah ameyasema hayo Mkoani Morogoro wakati akizindua mashindano ya Michezo ya Majeshi nchini yaliyoratibiwa na Baraza la Michezo ya Majeshi ya Tanzania (BAMMATA) na kufanyika hafla iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri.
Mhe. Hemed Suleiman amesema, michezo inasaidia kuimarisha afya lakini iwe chachu ya kupambana na kuzuia uharifu na matumizi ya dawa za kulevya ndani ya jamii kwa njia ya kuwashawishi wananchi hususan vijana kujiunga kwenye michezo ili kuepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu hususan ubakaji, wizi, ujambazi na matendo mengine yasiyokubalika katika jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BAMMATA Brigedia Jeneral Said Hamisi Said amesema mashindano hayo yatafanyika kwa siku 10 kuanzia Septemba 6 hadi 15, 2024 na kutaja michezo itakayochezwa katika mashindano hayo kuwa ni mpira wa Miguu, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mchezo wa riadha, mchezo wa ngumi, mchezo wa vishale na kulenga shabaha
Sambamba na hayo amebainisha Viwanja vitakavyotumika kwenye mashindano hayo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuwa ni viwanja vya Jamhuri, viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine – SUA, viwanja vya chuo cha Kijeshi cha Pangawe na viwanja vya Bwalo.