Nchini Ghana, polisi wamethibitisha kuwakamata waandamanaji 42 katika mji wa mkuu wa Accra, baada ya kutokea kwa makabiliano wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.
Waandamanaji wanalalamikia pia namna serikali kwenye taifa hilo inavyoshugulikia tatizo la uchimbaji haramu wa madini maarufu kama “galamsey”.
Maandamano hayo yalioanza siku ya Ijumaa ya wiki iliopita yalikuwa yanatarajiwa kuendelea hadi Jumatatu ya wiki hii.
Wengi wa waandamanaji hao ambao walikuwa ni vijana, wamesikika wakiimba nyimbo za kizalendo wakiwa wamebeba mabango yaliokuwa na maandishi kueelezea namna uchumi umeharibika kutokana kile wanachosema ni hatua ya serikali kushindwa kukabiliana na uchimbaji haramu wa madini.
Msemaji wa polisi Grace Ansah-Akrofi ameiambia AFP kwamba waliokamatwa walikuwa wamekusanyika bila kibali ambapo pia waliwashambulia polisi waliokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Polisi inasema waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mhakamani kujibu mashtaka mbalimbali ikiwemo kuharibu mali, kusababisha usumbufu sawa kuhitilafiana na usafiri wa watu.
Waandamanaji hao pia wanakabiliwa na makosa ya kuchukua ufungo za gari la polisi na kuzitupa pamoja na kuondoa vizuizi vya polisi na kutatiza amani ya raia.Viongozi wa maandamano hayo pia wanasakwa na polisi akiwemo wakili maarufu na mwanaharakati Oliver Barker-Vormawor.