Serikali ya Syria ilianguka mapema Jumapili katika mwisho wake wa kushangaza wa utawala wa miaka 50 wa familia ya Assad, baada ya mashambulizi ya ghafla ya waasi kuvuka eneo linaloshikiliwa na serikali na kuingia mji mkuu katika siku 10.
Televisheni ya taifa ya Syria ilirusha taarifa ya video ya kundi la wanaume wakisema kuwa rais Bashar al-Assad amepinduliwa na wafungwa wote waliokuwa jela wameachiliwa huru.
Mtu aliyesoma taarifa hiyo alisema chumba cha Operesheni cha Kushinda Damascus, kikundi cha upinzani, kilitoa wito kwa wapiganaji wote wa upinzani na raia kuhifadhi taasisi za serikali za “taifa huru la Syria.”
Wakaazi walionekana wakishangilia katika mitaa ya mji mkuu, huku makundi ya waasi yakitangaza kuondoka kwa “jeuri” Assad na “kutangaza mji wa Damascus kuwa huru.”
“Baada ya miaka 50 ya ukandamizaji chini ya utawala wa Baath, na miaka 13 ya uhalifu na dhuluma na (kulazimishwa) kuhama makazi … tunatangaza leo mwisho wa kipindi hiki cha giza na kuanza kwa enzi mpya kwa Syria,” vikundi vya waasi vilisema kwenye Telegram.