Watu wenye silaha wamewaua abiria 23 baada ya kuwatoa kwenye mabasi, magari, na malori katika shambulio moja la kikatili lililotokea katika eneo la Musakhail, mkoa wa Baluchistan kusini mwa nchi ya Pakistan.
Shambulio hili linatajwa kuwa moja ya mashambulio mabaya zaidi katika eneo hilo lenye machafuko. Polisi na maafisa wa serikali wameripoti leo kuwa washambuliaji walichoma moto magari angalau 10 kabla ya kutoroka eneo la tukio, katika tukio tofauti lililotokea leo asubuhi, watu wenye silaha waliwaua watu tisa, wakiwemo maafisa wanne wa polisi na wapita njia watano katika wilaya ya Qalat, Baluchistan.
Mashambulio mengine pia yameripotiwa katika sehemu mbalimbali za mkoa huo.
Wakati huo huo, waasi walilipua njia ya reli katika wilaya ya Bolan, mkoa huo, na kusababisha usumbufu mkubwa katika usafiri wa treni. Pia, walishambulia kituo cha polisi katika wilaya ya Mastung ingawa hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Aidha Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mohsin Naqvi, walilaani vikali shambulio la Musakhail na kuahidi kuwa wahusika hawataepuka mkono wa sheria.
Mashambulio hayo yalifanyika saa chache baada ya kundi la waasi la Baluch Liberation Army (BLA) kutoa onyo kwa watu kuepuka barabara kuu, huku wakiendelea na mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Hata hivyo, hakuna kundi lililodai kuhusika na mauaji hayo ya usiku.