Wabunge wanne wa CHADEMA waliokuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa amri ya mahakama wameachiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, huku wakipewa onyo kali kwamba wakikiuka tena masharti ya dhamana watafutiwa.
Wabunge hao ni, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amesema licha ya kwamba hakuridhika na maelezo yaliyotolewa na washtakiwa lakini hatua ya kuwafutia dhamana ni kali sana na hataki kufanya hivyo anataka kesi isikilizwe na iishe kwa wakati.
Pia Hakimu Simba amemtaka Msigwa na Heche kuhakikisha wanawaleta wadhamani wao katika tarehe nyingine itakayopangwa kesi hiyo.
Hakimu Simba amesema endapo washitakiwa hao watashindwa kuwaleta wadhamini wao watarudi ndani.
“Hiki kitendo mlifanya makusudi haiwezekani washitakiwa watano wafike kwa wakati na nyie wanne mshindwe kufika kwa wakati tena na wadhamini,”amesema.
Baada ya hapo kesi imeahirishwa hadi Novemba 26 hadi 29, 2019 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wafuasi wa CHADEMA na baadhi ya viongozi walianza kuwakumbatia washitakiwa hao na kuwapa pole.
Novemba 15, mwaka huu 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru wabunge hao wanne wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.
Amri ya kukamatwa kwa wabunge hao imetolewa na Hakimu Simba baada ya wabunge hao kutofika mahakamani hapo wakati kesi yao ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa bila kutoa taarifa yoyote na wadhamini wao pia kutokuwepo.
Washtakiwa waliofika mahakamani Novemba 15, 2019 ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji na Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko.
Katika Kesi hiyo Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.
Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.