Tovuti ya Israel ya Ynetnews imeripoti kuwa wadukuzi wa Iran wamefanikiwa kupenya kwenye mitandao ya makampuni zaidi ya 30 ndani ya utawala huo.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, kampuni ya usalama ya habari ya ESET imegundua kuwa wale iliowaita wadukuzi wa Iran wametumia fursa ya udhaifu uliopo katika seva za barua pepe za makampuni 32 ya Israel kuanzisha kile kiitwacho mlango wa nyuma, uliowaruhusu kujipenyeza kwenye mitandao ya makampuni hayo.
Kampuni moja ya usalama wa mtandao, ambayo imekataa kufichua majina ya makampuni yaliyodukuliwa imesema, wadukuzi hao wa Iran wamedukua pia kampuni nyingine moja nchini Brazil na nyingine katika Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makampuni yaliyodukuliwa yanafanya kazi katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na bima, dawa, viwanda, mawasiliano, IT, teknolojia, biashara za rejareja, magari, shughuli za kisheria, huduma za kifedha, usanifu majengo na uhandisi wa majengo.
Tovuti ya Ynetnews imeeleza kwamba kundi hilo la wadukuzi lilijitambulisha kwa jina la Ballistic Bobcat, ambalo pia linafahamika kwa majina mengine, likiwemo Charming Kitten, TA543 au PHOSPHORUS pamoja na APT35/42. Imeongeza kuwa, kuna makampuni mengine yasiyopungua 16 ambayo yamehujumiwa na wadukuzi wengine.